1. main content
  2. main navigation
  3. extra content
  4. head navigation
  5. search
  6. Choose form 30 Languages

 
 
 

 

 | 09.01.2009 | 04:00 UTC

Mswada wa azimio kutaka mapigano yasitishwe Gaza umeidhinishwa na Baraza la Usalama

NEW YORK:

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuunga mkono mswada wa azimio linalotoa mwito wa kusitisha moja kwa moja mapigano kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.Azimio hilo limepitishwa na nchi wanachama 14.Marekani imezuia kura yake.

Mswada wa azimio hilo uliopendekezwa na Uingereza na kuungwa mkono na Marekani na Ufaransa uliweza kupatikana baada ya kufanywa majadiliano marefu na makubaliano kupatikana kati ya wanadiplomasia wa nchi za Kiarabu na za Magharibi.Haijulikani kwa umbali gani Israel na Hamas zitatimiza masharti ya makubaliano hayo.

Miswada mingine iliyopendekezwa hadi hivi sasa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza ilipingwa na Marekani na Uingereza.


Lori la kusafirishia misaada ya Umoja wa Mataifa lafyatuliwa risasi na wanajeshi wa Israel katika Gaza

NEW YORK:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amelaani mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya mlolongo wa malori ya kupeleka misaada ya Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Gaza.Shirika la misaada limesitisha operesheni zake katika eneo hilo la mgogoro kwa sababu ya hatari inayosababishwa na vikosi vya Israel.Uamuzi huo ulipitishwa baada ya kuuawa kwa dereva mmoja baada ya lori lililokuwa likisafirisha misaada kufyetuliwa risasi na wanajeshi wa Israel.

Mkuu wa shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa,Antonio Gutteres amesema,vita hivyo ni mgogoro pekee duniani ambako watu hawaruhusiwi hata kukimbilia kwingine.Hadi hivi sasa,si chini ya Wapalestina 760 wameuawa katika mashambulizi ya vikosi vya Israel.Wanajeshi 8 wa Israel pia wameuawa.Vile vile maroketi yaliyorushwa na Hamas yameua raia 4 wa Kiisraeli.

Rais Mteule Obama aonya uchumi wa Marekani upo hatarini kuporomoka zaidi

WASHINGTON:

Rais Mteule Barack Obama ameonya kuwa Marekani inakabiliwa na hatari kwa uchumi wake kuzorota kwa miaka kadhaa ikiwa serikali haitochukua hatua za haraka.Alipozungumza katika Chuo Kikuu cha George Mason mjini Fairfax karibu na Washington Obama alisema,kuna hatari kwa idadi ya wakosa ajira kuongezeka na kufikia hadi tarakimu mbili.

O-TON OBAMA:

"Obama anasema,kwa wakati huu ni serikali peke yake inayoweza kuchukua hatua za muda mfupi zinazohitajiwa kupiga jeki uchumi ili kuinusuru nchi kutoka janga la hivi sasa.

Ameahidi kupunguza kodi ya mapato kwa familia zinazofanya kazi na kuzindua miradi itakayotoa nafasi mpya za kazi kwa takriban watu milioni tatu.Mpango huo wa msaada unajumuisha miradi ya kuwasaidia wakosa ajira na kuwapatia wananchi hao huduma za afya na vile vile kuzidisha maradufu uzalishaji wa nishati mbadala.Amesema,mpango wa kusaidia kufufua uchumi wa Marekani,utagharimu kama Euro bilioni 950.Barack Obama anaingia madarakani tarehe 20 Januari.

Kansela wa Ujerumani atoa mwito wa kuundwa baraza la uchumi duniani

PARIS:

Ulaya inashinikiza kufanywa marekebisho katika mfumo wa uchumi duniani.Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alipozungumza kwenye mkutano wa Uchumi wa Kimataifa mjini Paris alitoa mwito wa kuundwa baraza la uchumi duniani.Amesema,mkataba wa Umoja wa Mataifa wa uongozi wa uchumi enedelevu uwe msingi wa baraza la uchumi duniani.Kansela Merkel akaongezea kuwa Shirika la Fedha Duniani IMF na taasisi zingine za fedha zilizokuwepo,zimeshindwa kusimamia vizuri masoko ya fedha duniani.

Na rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy katika hotuba iliyoilenga Marekani amesema,katika karne ya 21 hakuna taifa moja pekee litakalokuwa na usemi.Amesema,hali hiyo haitorejewa tena.

Tume ya wasimamizi kuruhusiwa Ukraine katika mzozo wa gesi

PRAGUE:

Waziri Mkuu wa Urusi Vladimir Putin na mwenzake Mirek Topolanek wa Jamhuri ya Czech wametia saini masharti ya kuruhusu wajumbe wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya kusimamia usafirishaji wa gesi ya Urusi hadi Ulaya.Makubaliano hayo yametimiza dai kuu la Moscow na hivyo kufungua njia kwa kampuni kubwa ya gesi ya nchi hiyo Gazprom kuanza kusafirisha gesi hadi nchi za Ulaya kupitia Ukraine.Hapo awali Ukraine ilikataa kuruhusu tume ya wasimamizi.

Tangu majuma kadhaa Gazprom na kampuni ya gesi ya Ukraine Naftogaz zinazozana kuhusu madeni yasiolipwa na Ukraine kwa gesi ya Urusi na pia kuhusu bei ya siku zijazo.

Marekani yasema afisa wa ngazi ya juu wa Al Qaeda ameuawa Pakistan

WASHINGTON:

Maafisa wa Marekani wa kupambana na ugaidi wanaamini kuwa mkuu wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda nchini Pakistan ameuawa.

Ripoti zinasema,mkuu wa operesheni za kundi hilo,Usama al-Kini anaeaminiwa kuhusika na shambulizi la bomu lililofanywa dhidi ya hoteli ya Marriott mjini Islamabad ameuawa  pamoja na luteni wake.Hakuna habari zaidi zilizotolewa.

Afghanistan yasema raia wameuawa katika operesheni iliyoongozwa na Marekani

KABUL:

Majeshi shirika yanayoongozwa na Marekani nchini Afghanistan yameshutumiwa na Rais Hamid Karzai kwa mauaji ya raia 17 katika operesheni iliyolenga wanamgambo katika wilaya ya Laghman,mashariki mwa nchi.Karzai vile vile amewalaani wanamgambo kwa kuwatumia raia makusudi,kama kinga ya binadamu.

Maafisa wa jeshi la Marekani wanasema,ni wanamgambo tu waliouawa katika operesheni iliyolenga mtandao wa mabomu yanayozikwa kando ya barabara.Katika tukio jingine,raia 3 waliuawa na wengine 9 walijeruhiwa katika shambulizi la bomu la kujitolea maisha muhanga.Shambulizi hilo katika wilaya ya kusini ya Kandahar,lililenga mlolongo wa magari ya majeshi yaliyo chini ya uongozi wa NATO.



 
Picture of the Day
ImageOfTheDay

DW-TV EUROPE live

Journal (english) - With In Depth