| 03.12.2008 | 15:00 UTC
Safari za ndege zaanza kusafirisha watalii 350,000 waliokwama Bangkok
BANGKOK
Safari za ndege za kimataifa na zile za ndani ya nchi kutoka mji mkuu wa Thailand Bangkok zimeanza taratibu kuwasafirisha takriban watalii 350,000 kurudi makwao.
Waandamanaji wanaopinga serikali ya Thailand wameacha kuzingira viwanja vikuu viwili vya ndege mjini Bangkok leo hii asubuhi baada ya kuvizingira kwa juma moja.Wafuasi wa chama cha Muungano wa Wananchi kwa ajili ya Demokrasia waliahidi kukomesha maandamano yao dhidi ya serikali baada ya mahkama ya katiba nchini Thailand kumvua madaraka yake Waziri Mkuu Somchai Wongsawat na kukipiga marufuku chama tawala cha Madaraka ya Wananchi pamoja na vyama vengine viwili vilivyokuwa vikiunda serikali ya mseto kutokana na kufanya udanganyifu wa uchaguzi.
Mahkama hiyo pia imewapiga marufuku viongozi waandamizi wa chama hicho kushirikia katika siasa kwa miaka mitano.
Naibu Waziri Mkuu Chaowarat Channdeerakut ametangazwa kusimamia serikali ya mpito.







